Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) limepinga uamuzi wa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungia kwa muda usiojulikana vituo vya Magic FM na Radio 5.

Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye juzi alitangaza kuvifungia vituo hivyo kwa sababu za kukiuka kanuni za utangazaji na kurusha vipindi vyenye maudhui ya uchochezi.

Katibu wa Jukwaa la wahariri, Nevile Meena amekosoa uamuzi huo akieleza kuwa Waziri Nape hakueleza kiundani makosa ya vituo hivyo na kwamba hakutoa historia ya awali ya mwenendo wa vituo hivyo.

Amesema kwa muda mfupi aliokuwa Waziri ambaye ni mlezi wa vyombo vya habari ameshajitokeza mara nne kufuta na kufungia vyombo vya habari mbalimbali ikiwa ni pamoja na magazeti na majarida.

“Katika muda wa miezi takribani kumi tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa habari, Mh. Nnauye amejitokeza mara nne mbele ya vyombo vya habari kutangaza kufuta au kufungia vyombo vya habari,” amesema Meena.

“Alianza kulifuta gazeti la Mawio, baadae alitangaza kufuta mamia ya magazeti na majarida ambayo hayajachapishwa kwa muda mrefu, ikifuatiwa na adhabu ya kufungia kwa miaka mitatu gazeti la Mseto na sasa vituo viwili vya radio,” aliongeza.

Aliongeza kuwa  msimamo wa TEF unauona uamuzi wa Waziri Nape kuwa hauna nia njema na kwani kifungu alichotumia kuvifungia vituo hivyo vya radio havimlazimishi kufanya hivyo.

“Kosa la vituo hivyo kwa mujibu wa waziri ni uchochezi, lakini hakuweka bayana maudhui ya vipindi au habari ambazo zilifanya vituo hivyo kutiwa hatiani na baadae kufungwa kwa muda usiojulikana,” alisema.

 

Klabu Kadhaa Zaonyesha Nia Kwa Jack Wilishere
Yametimia, Joe Hart Amalizana Na Torino FC