Wakati Kikosi cha Simba SC kikitarajia kucheza mchezo wa pili wa Kirafiki kisiwani Unguja-Zanzibar kesho Jumatano (Septemba 28), Kocha Mkuu wa Muda wa Simba SC Juma Mgunda ametangaza kuiweka kiporo Primera de Agosto ya Angola.
Juzi Jumapili (Septemba 25) Simba SC tayari imeshacheza dhidi ya Malindi FC na kuibuka na ushindi wa 1-0, ukiwa mchezo wa kwanza wa Kirafiki tangu ilipowasili Zanzibar mwishoni mwa juma lililopita.
Kocha Mgunda amesema anafahamu Simba SC inakabiliwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Primera de Agosto, lakini anachokitazama kwa sasa ni mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma jiji FC.
Amesema michezo ya Kirafiki wanayocheza huko Zanzibar ina lengo la kuangalia mapungufu na mazuri ya kikosi chake, hatua ambayo itaendelea kumsaidia kuwaandaa wachezaji kuelekea mchezo unaofuata.
“Natumia michezo ya Kirafiki ili kuangalia mapungufu na mazuri ndani ya kikosi changu ili niweze kufanya maboresho, tutaanza kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma jiji, halafu tutacheza kimataifa dhidi De Agosto ya Angola,”
“Naamini michezo hii itaniongoza kujua wapi tunapaswa kuboresha na kukifanya kikosi chetu kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya ilivyokua katika michezo iliyopita, imani yangu ni kuwa tutakaporejea katika michezo ya kimashindano tunakuwa tofauti sana.”
“Kila mchezo unakua na maandalizi yake, kwa sasa tunaangalia kilicho mbele yetu, Dodoma Jiji ndio tutaanza nao halafu utafuata mchezo wa Kimataifa, kwa hiyo tunajiandaa na kilicho mbele yetu kwanza hayo mengine yatakuja baadae.” amesema Kocha Mgunda
Simba SC itacheza dhidi ya Dodoma Jiji FC Jumapili (Oktoba 02), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.