Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema ameiona na kuitathmini vizuri Ratiba ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kupangwa kwa Makundi ya Michuano hiyo.
Simba SC iliwafahamu wapinzani wake katika Michuano hiyo juzi Jumatatu (Desemba 12), baada ya kupangwa kwa Makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Kocha Mgunda ambaye ameweka Rekodi ya kuwa Kocha wa Kitanzania wa kwanza kuivusha Simba SC kutoka Hatua za awali hadi Hatua ya Makundi kwa kuzifunga Nyassa Big Bullet (Malawi) na Primeiro De Agosto (Angola), amesema yupo tayari kwa Michuano hiyo ya kimataifa.
Amesema anatambua ni mtihani mzito kwake kwa sababu atakua anakiongoza kikosi cha Simba SC kwa mara ya kwanza katika Hatua ya Makundi, lakini amesisitiza hana shaka na hilo kwa sababu ana wachezaji wengi wenye uzoefu wa kupambana Kimataifa.
“Hii ni mara yangu ya Kwanza kiushiriki hatua ya Makundi, lakini hilo halinishtuii kwa sababu wachezaji wangu wengi wana uzoefu wa kucheza Michezo ya Hatua ya Makundi, nitahakikisha tunajiandaa vizuri kwa usaidizi wa Uongozi, ili tuweze kufanya vizuri.”
“Tumepangwa katika Kundi gumu, nafahamu kuna baadhi ya Mashabiki wanaamini ni Kundi rahisi, lakini niwaambie tu katika Soka hakuna timu dhaifu hasa katika michuano hii, wote tumefika katika Hatua hii kutokana na ubora tuliouonesha, kwa hiyo nimelipokea Kundi letu kwa mikono miwili.”
“Nafahamu kiu ya Mashabiki ni kubwa kuiona timu yao inafanya vizuri na kutinga hatua inayofuata, kikubwa ninawaomba Mashabiki na Wanachama kuwa kitu kimoja na timu yao, kwa sababu huu ndio wakati wa kudhihirisha hilo, ili kuwawezesha wachezaji kupambana kwa moyo wao wote.” amesema Mgunda
Mara ya mwisho Simba SC iliishia hatua ya Robo Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, na kutolewa na Kaizer Chief ya Afrika Kusini kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3.