Kocha Mkuu wa Geita Gold FC Fred Felix Minziro ni kama ameshamkatia tamaa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazinkiza, kufuatia tetesi zinaoendelea kuelekea Dirisha Dogo la usajili, ambalo rasmi litafunguliwa usiku wa kuamkia kesho.

Simba SC inatajwa kuongoza katika mbio za kumuwania kiungo huyo ambaye aliwahi kucheza Soka la Kulipwa katika nchi za Uholanzi na Ufaransa kabla ya kutua Young Africans ya Tanzania.

Minziro amesema ni faraja kwake kama Kocha Mkuu kuona mchezaji anayemfundisha anahushwa na mpango wa kuwaniwa na zaidi ya Klabu moja katika msimu huu wa Dirisha Dogo.

Amesema suala hilo ni la kawaida kwa mchezaji yoyote duniani, kwa sababu muda unapofika kutoka klabu moja kwenda nyingine, huwa haliwezi kuzuilika kutokana na mahitaji ya Klabu iliyodhamiria kumsajili.

“Ni fahari kwa kocha kuona unamfundisha mchezaji kisha anatakiwa na timu nyingine, pia ni juhudi zake mwenyewe, amekuwa akizionyesha na zimemsaidia, ametokea Young Africans na sasa Simba SC imeonesha nia na kumuhitaji, pia kuna timu nyingine mbili ama tatu zote zinamuwania.”

“Yeye mwenyewe ndio ataangalia ofa yake aone anakwenda wapi kwa kuwa mwenye maamuzi ni yeye kuangalia wapi panamfaa ili aweze kwenda kujiunga.”

Saido alisajiliwa Geita Gold FC mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuachana na Young Africans mwishoni mwa msimu uliopita, hadi sasa amekua msaada mkubwa kwenye kikosi cha Minziro kwa kufunga mabao muhimu na kutoa pasi za mwisho.

Kocha Vipers SC azitisha Simba SC, Horoya AC, Raja
Juma Mgunda: Kundi letu ni gumu na zito