Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC wamekuwa wakwanza kufuzu hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kuichabanga AS Monaco ya Ufaransa mabao 2-1 katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali, uliochezwa kwenye uwanja wa Juventus Arena huko jijini Turin, Italia.

Mabao ya Juventus waliokuwa wanasaka rekodi ya kufuzu fainali kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu, yalifungwa na beki wa kutoka nchini Brazil Dani Alves na mshambuliaji kutoka nchini Croatia Mario Mandzukic. Bao la kufutia machozi upande wa AS Monaco, lilifungwa na kinda wa Kifaransa, Kylian Mbappe.

Ushindi huo umewafanya Juventus kufuzu hatua ya fainali kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa juma lililopita huko Stade Loius II mjini Monaco, Ufaransa.

Juventus watacheza fainali na mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya pili utakaochezwa leo siku kwa saa za Afrika mashariki, ambapo Real Madrid watakua ugenini wakiwakabili Atletico Madrid.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali, Real Madrid walishinda mabao 3-0.

Mchezo wa fainali wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya umepangwa kuchezwa Juni 3, mjini Cardiff, Wales.

Sadio Mane Adhihirisha Ubora Wake Anfield
?LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 10, 2017