Katika hali ya Mshangao Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Juventus ya Italia imetangaza kujiuzulu, akiwemo Rais Andrea Agnelli.
Maamuzi ya Bodi ya klabu hiyo kongwe katika Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ yamekuja kufuatia hasara ya Euro Milioni 254.3 sawa na Pauni Milioni 220 iliyopatikana, baada ya Juventus kumaliza Ligi msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya nne.
Novemba mwaka 2021, Uongozi wa Juventus ulitoa taarifa za kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini Italia, ili kupisha uchunguzi uliohusisha fedha za uhamisho wa baadhi ya wachezaji, ambazo zinadaiwa hazikupita katika mazingira halali.
Uchunguzi huo ulihusu mapato kutokana na haki za usajili wa wachezaji kati ya mwaka 2019 hadi 2021.
Agnelli na Makamu wa Rais Pavel Nedved, ambaye pia amejiuzulu, walikuwa miongoni mwa waliohusishwa na katika sakata la kuchunguzwa na Jeshi la Polisi nchini Italia, kuhusu matumizi ya Fedha za usajili.
Hata hivyo taarifa nyingine zinadai kuwa Bodi wa klabu hiyo ilifikia maamuzi ya kujiuzulu, kutokana na masuala ya kisheria na uhasibu yanayoendelea kuchukua mkondo wake kwa sasa.
Kwa maamuzi hayo Mkurugenzi Mtendaji Maurizio Arrivabene ataendelea na shughuli zake klabuni hapo, ili kuhakikisha mambo yanakaa sawa katika kipindi hiki cha mpito, hadi bodi mpya itakapoundwa.
Agnelli anakumbukwa kuwa mmoja wa waasisi wakuu wa mipango iliyojitenga ya kuunda kwa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya (European Super League) mwaka 2021.
Juve, ambao wameorodheshwa kwenye soko la hisa la Italia, wanachunguzwa kwa tuhuma za kuwasilisha taarifa za uhasibu za uongo kwa wawekezaji na kutoa ankara za miamala ambayo haipo.
Klabu hiyo imekana kufanya makosa yoyote.
Vilabu vingine pia vinahusika na uchunguzi sambamba ambao ulizinduliwa na Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) mnamo Oktoba.
Wanahisa wamepangwa kukutana tena tarehe Januari 18 mwaka 2023, ili kuteua bodi mpya, klabu hiyo.