Mabingwa wa Soka nchini Botswana Jwaneng Galaxy, wametuma salamu kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika utakaozikutanisha timu hizo mwishoni mwa juma hili.

Jwaneng Galaxy, wataanzia nyumbani Oktoba 17, kabla ya kumaliza mchezo wa mkondo wa pili Uwanja wa Benjamin mkapa, jijini Dar es salaam Tanzania Oktoba 22.

Mkuu wa Benchi la Ufundi la Jwaneng Galaxy, Morena Ramoreboli, amesema wamedhamiria kuishangaza Afrika kwa kuibamiza Simba SC katika michezo hiyo miwili, ili watinge kwenye hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo ya Botswana.

Morena amesema anaamini suala hilo linawezekana, licha ya kukiri Simba SC ni klabu kubwa, katika ukanda wa Bara la Afrika, baada ya kuonesha maajabu kwenye michuano Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

“Ninaheshimu sana uwezo wa Simba ambao wameuonesha katika miaka ya hivi karibuni, katika michuano ya kimataifa wamefika hatua nzuri, ni timu kubwa, hivyo tunatakiwa kupambana haswa ili kutimiza malengo yetu ambayo ni kusonga mbele.”

“Tunayo faida ya kuanzia nyumbani, hivyo tunatakiwa kufanya vizuri katika mchezo wetu wa mwanzo, tutapambana kuhakikisha tunasonga mbele, hakuna namna nyingine zaidi ya kwenda kupambana na Simba.” amesema Morena.

Msimu wa 2020/21 Simba SC ilifika hatua ya Robo Fainali na kuondoshwa kwenye michuano hiyo kwa kufungwa mabao 4-3 na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Jwaneng Galaxy, ilipenya katika hatua ya awli na kutonga hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kufuatia kuibamiza DFC Sème ya Jamhuri ya Afrika ya Kati juma la mabao 2-1.

Sakho hatarini kuikosa Jwaneng Galaxy
Wachimbaji 175 wafutiwa leseni