Kukamilika kwa mradi wa umeme wa Rusumo wa megawati 80, kutaimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kumekuwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa Nishati hiyo pungufu huku Mkoa wa Kagera nao ukitarajia kuanza kutumia umeme wa gridi.

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema hayo akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani Ngara Mkoani Kagera, wakati alipokagua kazi ya ujenzi mradi huo wa ubia baina ya nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi kabla ya kuzungumza na Wananchi.

“Katika kipindi cha miezi Sita iliyopita tumefanya kazi kubwa ya kusukuma na kushirikiana na wenzetu ili kuhakikisha kwamba unakamilika haraka, tunautegemea mradi huu utaongeza uwezo, nguvu na uhakika wa umeme katika Kanda ya Ziwa,” alisema Makamba.

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Wananchi.

Kuhusu ujenzi wa njia ya kusafirisha kutoka eneo la mradi hadi Nyakanazi, Waziri huyo wa Nishati amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi ili umaliziaji wa miundombinu ya kuchukua umeme kwenye mradi wa Rusumo uendane ule wa mitambo ya kuzalisha umeme.

Makamba pia amekagua eneo kutakapojengwa kituo cha kupoza umeme na kuitaka TANESCO kuharakisha ujenzi wa kituo hicho kitakachotoa umeme kutoka mradi wa Rusumo na kuusafirisha kwa msongo wa kV 220 kwenda Kyaka mkoani Kagera ambao unatarajia kupata umeme kutoka gridi ya Taifa.

Kuhusu, malalamiko ya fidia kwa kaya 1200 zilizoathirika kutokana na kufunga njia kubwa ya maji ili kuetekeleza mradi wa umeme wa Rusumo, Waziri amesema zilizothibitishwa hadi sasa ni 1,041 na watalipwa fidia hiyo Septemba 2022 huku nyumba 304 zilizoathiriwa na shughuli za ujenzi huo zikiwa na uhakika wa kukarabatiwa.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba pia akihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi kwa mmoja wa Mama Lishe aliyekuwa akitumia kuni na mkaa kupikia.

Licha ya kukagua miradi ya umeme katika Wilaya ya Ngara, Karagwe na Misenyi mkoani Kagera, Waziri Makamba pia amehamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kugawa mitungi ya gesi 200 kwa vikundi vya Mama Lishe waliokuwa wanatumia kuni na mkaa kupikia.

Mradi huo, unaohusisha ujenzi wa mtambo wa uzalishaji umeme, bwawa, eneo la kupokea umeme kabla haujasambazwa na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi hadi Nyakanazi, umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.

Jemedari Said amvaa tena Haji Manara
Kocha Zoran Maki awekewa mtego Simba SC