Takriban watu 193 wakiwemo watumishi wa afya, ambao waliochangamana na wagonjwa wa ugonjwa wa Marburg katika Mkoa wa Kagera wamewekwa karantini kwa ajili ya kufatiliwa maendeleo yao ya kiafya ambapo kati ya watu waliowekwa karantini, 89 ni watumishi wa afya na 104 ni kutoka kwenye jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Machi 23, 2023 juu ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali kudhibiti ugonjwa huo, Mganga Mkuu wa Serikali nchini Prof. Tumaini Nagu amesema wanaendelea kufuatilia watu waliotengamana na wagonjwa hao.
Amesema, “tunaendelea kuwafatilia na hawa wagonjwa na mpaka sasa tunao watu 193 ambao wametangamaa na ugonjwa huu wa Marburg na kati yao 89 ni watumishi wa afya na 104 wako kwenye jamii, lakini mpaka sasa hakuna aliyeonesha dalili za ugonjwa wa Marburg kati ya hao.”
Aidha Dkt. Nagu ameongeza kuwa mpaka sasa ugonjwa umedhibitiwa na kuikumbusha jamii kuhusu dalili za ugonjwa huo, uliotangazwa na Waziri wa Wizara ya Afya, Ummy Mwalimu March 21,2023 ambaye aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.