Klabu ya Real Madrid inamfukuzia mchezaji wa Chelsea raia wa Ujerumani, Kai Havertz katika dirisha hili kubwa majira ya joto ili kuhakikisha wanaimarisha kikosi chao katika safu ya ushambuliaji.
Real Madrid inahitaji mshambuliaji mwingine ili kuboresha timu hiyo kwenye safu ya ushambuliaji na Havertz ameingia kwenye orodha ya wababe hao wa soka nchini Hispania.
Klabu hiyo inafikiria kutuma ofa kwa klabu ya Chelsea kwa ajili ya kumpata mchezaji huyo huku Chelsea ikiwa tayari kumwachia baada ya msimu wa 2022/23 kumalizika.
Klabu hiyo ya jijini London imeweka bayana kuwa itamuuza jumla na suala la kutolewa kwa mkopo sio kipaumbele chao hivo wako tayari kusikiliza ofa kwa klabu ambazo zitakua zinamtaka mchezaji huyo.
Real Madrid wao watatuma ofa kwa klabu ya Chelsea lakini inafahamika kuwa klabu hiyo haipo tayari kutoa dau kubwa kumnunua mshambuliaji huyo, kwani mchezaji pekee ambaye wamepanga kumsajili kwa gharama kubwa ni kiungo wa kimataifa wa England, Jude Bellingham ambaye anakipiga kule Borussia Dortmund.
Taarifa za mshambuliaji Karim Benzema kuondoka klabuni hapo na kutimkia Saudia Arabia zimeifanya klabu hiyo kuanza kutafuta mshambuliaji mwingine haraka.