Mlinda Lango wa Young Africans, Djigui Diarra amehuzika baada ya timu yake kushindwa kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Barani Afrika licha ya kutangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mchezo wa Fainali.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara walishindwa kutwaa taji hilo kwa kanuni ya bao la ugenini, licha ya kushinda mechi ya marudiano kwa bao 1-0 mjini Algiers juzi Jumamosi (Juni 03) baada ya kupata kipigo cha mabao 2-1 nyumbani jijini Dar es salaam Jumapili (Mei 28).

“Tulijitolea kwa kadri tulivyoweza na kwa juhudi sana. Kwa bahati mbaya, haikutosha. Tuliota taji hili na tulistahili kushinda. Lakini hatima haikuturuhusu,” amesema mchezaji huyo wa kimataifa wa Mali

Diarra alitajwa kuwa Mchezaji bora wa mchezo huo, kufuatia kuonyesha kiwango kikubwa huku kupangua mkwaju wa penalti dakika ya 59 na sambamba na kufanya kazi kubwa ndani ya dakika zote 90.

“Nina furaha sana kuwa mchezaji bora wa mechi ya fainali. Ni heshima kubwa kwangu. Ingekuwa bora kama na kombe tungetwaa, lakini haikuwa. Ninajivunia wachezaji wenzangu na kikosi kizima. Tulicheza kwa kiwango kizuri,” amesema Diarra.

Ameahidi kuwa watajitahidi kuwa katika hali kama hiyo msimu ujao, kwani wamepata uzoefu wa kutosha na njaa ya kufanikiwa imeongezeka.

“Tutarudi kwa nguvu na kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi. Tuna uzoefu na wachezaji wanataka kuja katika safari hii tena,” amesema mchezaji huyo.

Msimu ujao 2023/24 Young Africans itashiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ikipata nafasi hiyo baada ya kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo msimu huu 2022/23.

Kai Havertz awekewa mitego Santiago Bernabeu
Uwekezaji, Biashara EAC: Vikwazo vipya vinne vyawasilishwa