Beki wa kati wa KMC FC, Andrew Vincent ‘Dante’ amesema anajua ugumu wanaoenda kukutana nao kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, lakini wachezaji wote wamejipanga na kusema liwalo na liwe kwa vile kiu yao ni kushinda ili wajiweke schemu salama kukwepa kushuka daraja.

Nahodha msaidizi huyo wa KMC na aliyewahi kutamba na timu za Mtibwa Sugar na Young Africans amesema kikosi chao kina morali kubwa na wachezaji hawataki kuona timu hiyo ikishuka daraja kwani itakuwa ni rekodi mbaya kwa mchezaji mmoja mmoja katika maisha yake ya soka.

“Tunajua kabisa mchezo utakuwa mgumu na sio huu, bali hata ule wa mwisho lakini tupo kwenye kuipambania timu na hata sisi tusiwe na rekodi mbaya,” amesema Dante na kuongeza;

“Pia, kitendo cha kufika Sumbawanga mapema na kuzoea hali ya hewa ya baridi ni jambo zuri tofauti na tungechelewa kufika ingetupa shida, kwa sasa angalau kidogo.” Amesema Dante ambaye amekuwa na wakati mzuri katika misimu mitatu mfululizo akiwa na KMC FC.

Maafande wa Tanzania Prisons kesho Jumanne (Juni 06) watawakaribisha KMC FC kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Mjini Sumbawanga, Rukwa baada ya timu hiyo kuhamishia maskani yake huko, huku ikiwa nafasi ya nane na alama zake 34, tano zaidi na ilizonazo KMC iliyopo nafasi ya 13.

Tayari Ruvu Shooting imeshashuka daraja na sasa zinatafutwa timu mbili za kuungana nayo katika Ligi ya Championship msimu ujao, ikiwamo itakayoshuka moja kwa moja ili kuzipisha JKT Tanzania na Kitayosce zilizopanda daraja kuliamsha Ligi Kuu msimu ujao. Timu nyingine itacheza play-off kuchuana na Mashujaa.

Uwekezaji, Biashara EAC: Vikwazo vipya vinne vyawasilishwa
TAWA: Majangili wapewa onyo takwimu zatolewa