Viongozi waliokutana katika mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Lusaka, Zambia wameahidi kuunga mkono mpango wa ‘Education Plus’ wakijitolea kuchukua hatua ya kuwafanya wasichana kubaki shuleni, jambo ambalo litapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wao wa kuambukizwa Virusi Vya UKIMWI, VVU.
Katika taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS iliyotolewa jijini Lusaka, Zambia na Geneva, Uswisi, imesema Kila wiki, takriban wasichana 4,200 na wanawake vijana katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hupata VVU.
Mwaka 2020, vijana sita kati ya saba wenye umri wa kati ya miaka 15-19 waliopata VVU katika eneo hilo, walikuwa wasichana ambapo zaidi ya wanawake vijana 23,000 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI mwaka 2020, na kuifanya kuwa sababu ya pili ya vifo kati ya wanawake wenye umri wa miaka 15-29 baada ya vifo vya uzazi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Taarifa hiyo imesema ili kuwafanya wasichana wabaki katika shule za upili au sekondari na kuwapa stadi za maisha, mafunzo na fursa za ajira ni muhimu katika kumaliza janga la UKIMWI barani Afrika.
Utafiti wa UNAIDS unaonesha kuwa kuhakikisha kuwa wasichana wanamaliza elimu ya sekondari kunapunguza hatari ya kupata VVU kwa hadi nusu, na kwamba kuchanganya hii na mfuko wa huduma na haki za uwezeshaji wa wasichana kunapunguza hatari yao bado.
Education Plus inataka elimu ya sekondari iwe ya bila kulipia na bora kwa wasichana na wavulana wote katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ifikapo mwaka 2025, upatikanaji wa elimu ya kina ya ujinsia kwa wote, utimilifu wa afya na haki za ngono na uzazi, uhuru dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kingono, mabadiliko ya kutoka shule hadi kazini na uhakika wa kiuchumi na uwezeshaji.
UN yataka uchunguzi vifo 23 vya Waafrika
Mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema amesema, “Serikali yangu imejitolea kutoa elimu ya bure ya msingi na sekondari kwa wote, elimu ni kitu muhimu cha kuleta usawa mkubwa na kwa elimu ifaayo, kila mtu anapewa fursa ya kuchunguza uwezo wake kamili na kuweza kushiriki katika mchakato wa maendeleo.”
Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, Macky Sall akizindua mpango huo akiwa na marais wengine watatu na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema mpango wa Education Plus umechukua uharaka zaidi kutokana na janga la Uviko-19 na kuwaacha mamilioni ya wasichana nje ya shuleni.
Hata kabla ya janga hili, karibu wasichana milioni 34 waliobalehe wenye umri wa miaka 12 hadi 17 katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hawakuwa katika shule za sekondari.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima, katika hotuba yake kwenye uzinduzi huo amesema, “tunapiga hatua barani Afrika lakini hatuna kasi ya kutosha. Tunahitaji kushughulikia kwa haraka ukosefu wa usawa wa kijinsia ambao bado unasumbua bara la Afrika, na athari mbaya kwa wasichana maskini na wanawake vijana. Hatuna dakika ya kusubiri.
Nchi kumi za Afrika – Benin, Cameroon, Eswatini, Gabon, Gambia, Lesotho, Malawi, Sierra Leone, Afrika Kusini na Uganda, hadi sasa zimejitolea kutekeleza mpango huo ambao umeitishwa kwa pamoja na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa, UNAIDS, UNESCO, UNFPA, UNICEF na UN Women, na unaleta pamoja serikali, mashirika ya kiraia na washirika wa kimataifa.