Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka Askari Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, kusimamia sheria kikamilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia ambao hufariki, kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizindua kongamano la kitaifa la wadau wa usalama barabarani nchini, ambapo amesema kuwa wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa.

“Usalama Barabarani unaanza na kila mmoja wetu, nawaomba sana tutumie fursa hii kikamilifu kwa kutoa mawazo na maoni yetu katika kongamano hili kwa manufaa na mustakabali wa Usalama wetu hivi sasa na vizazi vijavyo,” amesema Lugola.

Amewataka wadau hao, watumie fursa ya kongamano hilo kuzungumza kwa uwazi, kutoa mawazo yao ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa Baraza Usalama Barabarani na vyombo vingine ambavyo vinasimamia Sheria ya Usalama Barabarani.

Aidha, amesema kuwa Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kutokomeza ajali za barabarani nchini, hivyo amewataka wadau wa usalama barabarani wajipange kikamilifu kwa kuweka mikakati thabiti kwa lengo la kutokomeza ajali nchini.

Pia Waziri Lugola amelitaka Baraza la Usalama barabarani kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Baraza Awamu ya Nne, ambao umezinduliwa Waziri huyo ameuzindua na Muongozo wa Utendaji na Utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya ili kudhibiti ajali za Barabarani na Kuimarisha Utendaji wa Kamati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masuani amesema kuwa takwimu za usalama barabarani zimepungua nchini kutokana na Baraza lake kuweka mikakati za kupambana na ajali nchini.

 

Waziri wa Nishati apiga marufuku mgao wa Umeme
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Machi 31, 2019