Beki wa Kulia wa Simba SC Shomari Kapombe amesema wapo tayari kwa mchezo wa kesho Jumanne (Machi 07) dhidi ya Vipers SC, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa Mzunguuko wanne wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku ikishinda mchezo uliopita dhidi ya Vipers SC iliyokua nyumbani kwao Entebe-Uganda mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kapombe amesema wanakwenda katika mchezo huo wakiwa wanatambua umuhimu wake, hivyo kila mchezaji yupo tayari kwa kupambana na kuipa matokeo mazuri Simba SC.
Amesema wanatambua Vipers SC itacheza tofauti na ilivyokua kwenye mchezo uliopita, huku wakitumia mfumo wa kushambulia kwa kuhstukiza, lakini wajiandaa kwa kujifunza mbinu za kuwakabili na kuhakikisha wanashinda.
“Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu wa kesho, tumejipanga kupambana ili kupata ushindi katika Uwanja wetu wa nyumbani, tupo tayari kwa kila kitu, tunatarajia kushinda dhidi ya Vipers SC.”
“Tunafahamu watacheza tofauti huku wakipanga kushambulia kwa kushtukiza, tayari tumeshajiandaa kukabiliana nao kwa hali zote, ninaamini kwa maandalizi tulioyafanya yatatuwezesha kuwafunga kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita.”
“Mahabiki wetu wanapaswa kuja kwa wingi uwanjani kutupa nguvu na sisi tunawaahidi hatutawaangusha.” amesema Kapombe.
Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo wa kesho ikiwa na alama tatu mkononi, baada ya kuifunga Vipers SC nyumbani kwao, huku ikitangulia kupoteza michezo miwili dhidi ya Horoya AC ya Guinea na Raja Casabanca ya Morocco.
Vipers SC inaburuza mkia wa Kundi C ikiwa na alama 01, ikitanguliwa na Simba SC yenye alama 03, Horoya AC ipo nafasi ya pili kwa kumiliki alama 04, huku Raja Casablanca ikiongoza kundi hilo kwa kufikisha alama 09.