Mlinda Lango Mkongwe Juma Kaseja amesema hafikirii kustaafu Soka kwa sasa, na badala yake anasubiri ofa ya klabu yoyote katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili msimu huu 2022/23.
Kaseja ametoa kauli hiyo baada ya kuthibitika ameachana na KMC FC, kufuatia mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita na sasa amekuwa mchezaji huru.
Mlinda lango huyo ambaye amewahi kutamba na Klabu za Simba SC na Young Africans amesema, amekua akipokea ujumbe kutoka kwa Mashabiki wengi wa Soka wanaoulizia hatma yake kwa sasa, lakini amekua akiwajibu bado yupo na ataendelea kuonekana Dimbani kama atapata timu itakayomsajili.
Amesema asilimia kubwa ya Mashabiki wanaowasilina naye wamekua hawaamini kama ameachana na KMC FC, licha ya orodha ya wachezaji waliosajiliwa klabuni hapo kutangazwa hadharani, lakini amekua akiwathibitishia hilo.
“Watu wengi walikuwa hawataki kuamini kama sipo KMC FC, walipotangaza kikosi chao jina langu halikuwepo, kwa kuwa mkataba wangu ulikuwa umekwisha, ninaendelea na maisha mengine, kwa sasa mimi ni mchezaji huru,”
Hata hivyo Kaseja amesema yupo tayari kusajiliwa na klabu yoyote katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili ambacho kitafungwa rasmi mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema klabu yoyote hata ya Ligi Daraja la Kwanza itakayokua tayari kufanya naye kazi, hatasita kujiunga nayo, lakini jambo la msingu ni kufikiwa kwa makubaliano ya kimaslahi.
“Nitacheza timu yoyote itakayohitaji huduma yangu, hata ikiwa Ligi Daraja la Kwanza, tukiafikiana nitacheza.” amesema Kaseja
Mbali na Klabu za Simba SC, Young Africans na KMC FC, Kaseja pia amezitumikia klabu za Mbeya City na Kagera Sugar zote la Ligi Kuu Tanzania Bara.