Kasi ya rais John Magufuli aliyoianzisha ya kufanya ziara za kushtukiza iliyorithiwa na mawaziri aliowateua imemkuta tabibu maarufu wa tiba asilia za uzazi, Dk. Juma Mwaka wa Fore Herbal Clinic iliyopo jijini Dar es Salaam.

Dk. Mwaka alitimua mbio pamoja na wahudumu wake wa afya baada ya naibu waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, watoto na wazee, Dk. Hamisi Kigwangalla kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo chake cha afya.

Baada ya kuwasili katika kituo hicho, Dk. Kigwangalla alikuta mhudumu wa mapokezi na wateja wachache. Alieleza kufahamu mbinu aliyotumia Dk. Mwaka na wahudumu wake kumkimbia.

“Tunafahamu alikuwepo hapa na akajua kwamba tunakuja, na ameingia kwenye gari dakika kumi kabla sisi hatujafika hapa. Lakini la pili, tunafahamu walikuwepo matabibu, walikuwepo watu wa vipimo, tukiwa hapahapa lakini wote mmewatorosha kupitia mlango wa nyuma,” alisema Dk. Kigwangalla.

Dk Hamisi Kigwangala

Naibu waziri huyo aliongeza kuwa Dk. Mwaka anafanya makosa ya kujiita Daktari wakati hana vyeti vinavyoonesha kuwa yeye ni daktari na kwamba hata kujitangaza kwenye vyombo vya habari huhusu utoaji tiba ni kinyume cha miiko ya udaktari na utabibu.

Aidha, Dk. Kigwangalla alitoa siku nne pekee kwa Dk. Mwaka kujisalimisha na kufika ofisini kwake akiwa na vyeti pamoja na vielelezo vyote vinavyompa kigezo cha kuendesha huduma hiyo.

“Kwa sababu kuna mambo ambayo yanaendelea na wananchi wanalalamika kwenye jamii. Kwanza anajiita Doctor wakati hana cheti cha kusomea udaktari, pili anatumia mambo yanayoendana na taaluma ya udaktari wa kisasa kinyume cha taratibu,” alisema.

Kufuatia hatua hiyo, alimuagiza Mpelelezi msaidizi wa tiba asilia Dk. Paul Mohamed kufanya uchunguzi kuhusu huduma anazozitoa Dk. Mwaka na kuwasilisha majibu ndani ya wiki moja ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Kubenea Atiwa Mbaroni kwa Amri Ya Makonda, adaiwa kumkosea adabu
TFF Yavikumbusha Vilabu Kuheshimu Na Kufuata Taratibu