Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo Pauline Gekul amelitaarifu bunge kuwa shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania TFF na Kamati ya Olimpiki Tanzania TOC hazijawahi kubadili katiba zao kwa lengo la kuwalinda viongozi walioko madarakani.
Naibu Waziri Gekul amekanusha madai hayo leo bungeni, Baada ya swali la mbunge wa Makunduchi, Ravia Faina kuuliza kwanini? Vyama vya michezo vimekuwa vikibadili katiba zao kulinda viongozi walioko madarakani na kudhibiti watanzania wengine wasigombee nafasi katika vyama hivyo.
“Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba shirikisho la TFF na TOC hayajawahi kubadili katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi walioko madarakani, kwa kuwa mabadiliko yoyote ya kikatiba lazima yakidhi vigezo vya usajili vinavyosimamiwa na msajili wa vyama na vilabu vya Michezo nchini vikiwemo utawala bora na ukomo wa muda wa uongozi chini ya BMT,” amesema Naibu waziri Gekul
Aidha amezungumzia juu ya ukomo wa uongozi katika baadhi ya vyama vya michezo amesema kwa upande wa TOC tiyari suala hilo lilishafanyiwa marekebisho nakupelekwa kwa msajili huku akiahidi kutembelea kwenye ofisi za baadhi ya vyama ili kupitia vigezo vilivyopo na kuvifanyia kazi.