Chama cha Walimu Tanzania – CWT, kimesema mgogoro unaoendelea ndani yake unasababishwa na Katibu Mkuu, Japhet Maganga ambaye haheshimu taratibu za uendeshaji wa chama na miongozo yake.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma Naibu katibu Mkuu wa CWT, Joseph Misalaba amesema Kiongozi huyo amekuwa akifanya mambo kwa utashi binafsi kitu ambacho ni kinyume na taratibu.
Amesema, “yeye anatumia utashi binafsi na yapo mambo mengi ambayo kamati ya utendaji Taifa wameazimia kwenye vikao wakamshauri lakini amekuwa akikaidi kwa kutumia nafasi yake ya ukatibu Mkuu na kutumia njia haramu kutumia njia mbadala katika vikao vya chama.”
Aidha, Misalaba ameongeza kuwa kitendo alichofanya Katibu huyo Mkuu wa CWT Juni 6, 2023 cha kufunga mageti kwa mamlaka yake ni utovu wa nidhamu kwa Waliomuajiri (Walimu).
“Kiongozi kuendekeza vinyongo na visasi dhidi ya kiongozi yoyote ambae anahisi hamuungi Mkono au kumuunga Mkono hapo awali na kutoa huduma za chama kwa ubaguzi hakifai,” amefafanua Misalaba.
Hata hivyo amesema yapo maeneo mbalimbali ambayo yamekiukwa na katibu huyo kwenye kanuni za miongozo mbalimbali ikiwemo toleo la Nne la Mwaka 2015 kifungu cha 32 juu ya utatuzi wa Migogoro na nidhamu kwa viongozi.
“Kavunja katiba ya chama ibara ya 111 kifungu cha 22.3(f) kwa yeye kuandaa ajenda ya baraza la Taifa ya KUT, ametumia madaraka vibaya na amekaidi maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kazi Vijana na ajira na wenye ulemavu,” amesema.