Idara ya ufuatiliaji na tathmini ya utendaji, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, inakabiliwa na jukumu kubwa la kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa sera, mipango, programu, miradi na mikakati mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Serikali.

Hayo yamesemwa hii leo Juni 9, 2023, na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga wakati akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo ambao pamoja na mambo mengine, ulijadili tathmini na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali pamoja na kongamano la wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini  na mafunzo itakayofanyika mapema Septemba, 2023.

Amesema, baada ya Serikali kufanya maboresho ya Muundo wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) 2022/23,  Idara hiyo  mpya iliyoanzishwa, ndiyo inahusika moja kwa moja na kuandaa taarifa za utendaji wa Serikali za kila robo mwaka, nusu mwaka na taarifa za mwaka ikiwemo taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa ndani ya Taasisi za Umma na utekelezaji wa Malengo ya kimataifa na kikanda  na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika. 

Aidha, Naibu Waziri ameongeza kuwa, taarifa ya mwaka ya utendaji wa Serikali itakuwa ikisomwa Bungeni kuanzia mwaka ujao wa fedha (2023/24) ili kutoa taswira halisi ya uwazi na uwajibikaji wa Taasisi zote za Serikali kwa Wananchi na kusema, “ili kuwezesha Ofisi kupata taarifa hizi, itakuwa inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa viashiria vya utendaji kazi na kutoa taarifa katika ngazi mbalimbali.”

Awali, Naibu Waziri Nderiananga alisema kuwa Ofisi hiyo ipo maandalizi ya Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 12 – 15 Septemba, 2023 Mkoani Arusha.

Kongamano hilo litawaleta  pamoja, wadau wa maendeleo wa ufuatiliaji na tathmini ya Utendaji kazi ili kupashana habari na kupeana uzoefu wa namna ya kusimamia utekelezaji wa mipango, programu na miradi mbalimbali na kuonesha namna inavyosaidia jamii.

Serikali Wafanyabiashara wajadili ukuzaji wa masoko
Rasmi Sadio Mane anasepa Bayern Munich