Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza amesema kuwa alishtushwa na taarifa za kusitishwa kwa kilele cha Tamasha la Fiesta jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Jumamosi usiku mkoani Mtwara alipohudhuria Tamasha la Wasafi, Mngereza alisema amefurahishwa na ongezeko la matamasha nchini na kwamba siku hiyo kulikuwa na matamasha mawili makubwa pamoja na show moja, hali ambayo inaongeza ajira na pato la taifa.
“Mimi nilikuwa nafuraha ya juu sana kuona Mtwara (Nangwanda Sijaona) kuna Tamasha, na Dar es Salaam kuna tamasha la Fiesta ambalo wanafikia kileleni. Na Kahama, show ya Ali Kiba kwa sababu lile sio tamasha,” Mngereza aliiambia Bongo5.
“Mimi mwenyewe nimepata hamaki kuona kwamba tamasha la Fiesta limeahirishwa kwa sababu za msingi ambazo zimeelezwa. Lakini Baraza bado hatuna taarifa rasmi. Lakini kiukweli na mimi nimepata shock (mshtuko) kwa sababu ya hizo faida nilizokuwa naziangalia,” aliongeza.
Amefafanua kuwa faida ambazo zimepatikana Mtwara kwa wasanii, wafanyabiashara hadi dereva wa Bodaboda, pamoja na pato kwa Serikali zingepatikana katika mikoa yote mitatu kwa usiku mmoja.
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilitoa katazo la tamasha la Fiesta kufanyika katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam saa chache kabla ya kuanza kwa tamasha, na kuelekeza tamasha hilo lifanyike katika viwanja vya Tanganyika Packers vilivyoko Kawe.
Kutokana na maelekezo hayo yaliyotolewa wakati waandaaji wa Tamasha hilo, Clouds Media Group walikuwa wameshafunga jukwaa na kuandaa eneo hilo, walitangaza kuahirishwa kwa kilele cha tamasha hilo.