Baada ya kuisambaza Geita Gold FC kwa mabao 3-1, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amefichua siri ya mafanikio ambayo yameipa furaha klabu hiyo.
Mtibwa Sugar ilicheza nyumbani Manungu Complex mkoani Morogoro Juzi Alhamis (Oktoba 26), na kupata ushindi huo ambao unakuwa wa kwanza msimu huu 2023/24, chini ya kocha huyo aliyechukuwa nafasi ya Habib Kondo.
Katwila amesema ubunifu na utulivu uliooneshwa na wachezaji wake katika mchezo huo ndio siri ya ushindi waliopata dhidi ya Geita Gold.
Katwila amesema aliwaambia wachezaji wake kuwa watulivu hata kama watatanguliwa kufungwa maelekezo ambayo amesema waliyazingatia.
“Nimshukuru Mungu kwa kupata alama mbele ya mchezo mgumu kama ule, tulikuwa kwenye wakati mgumu wa kukosa matokeo, lakini niliwaambia wachezaji watoe hofu, wawe watulivu na kushambulia na hatimaye tulishinda,” amesema
Amesema baada ya kurejea Mtibwa alianza kufanyia kazi maeneo ya ushambuliaji, kiungo na ulinzi lengo likiwa kupata muunganiko mzuri anbao ungewasaidia kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao.
Kwa ushindi huo Mtibwa Sugar imefikisha alama 05 zinazoiweka katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.