Kocha mpya wa klabu ya Young Africans Cedric Kaze ameanza safari ya kuja nchini Tanzania akitokea Canada, tayari kwa kuanza majukumu yake ndani ya klabu hiyo.
Kaze alithibitishwa na viongozi wa Young Africans, baada ya kocha Zlatko Krmpotic kusitishiwa mkataba wake, mwanzoni mwa mwezi huu, kufuatia falsafa yake kushindwa kufanya kazi kikosini, licha ya kuibuka na ushindi kwenye michezo minne na kupata sare mmoja.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli, amethibitisha kocha huyo kuwa safarini kuja Dar es salaam – Tanzania, huku akeleza mapema leo alikuwa jijini Amsterdam Uholanzi, kwa ajili ya kubadilisha ndege.
Kaze anatarajiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere majira ya saa nne usiku leo kwa ndege ya Shirika la Ndege la KLM.
Awali kocha huyo kutoka nchini Burundi ilipaswa kujiunga na Young Africans Agosti 25 kurithi mikoba ya Luc Eymael raia wa Ubelgiji, ambaye alifutwa kazi, lakini ilishindikana kwa kuwa aliweka bayana kwamba anahitaji muda wa majuma mawili kutatua matatizo ya kifamilia.
Kaze ana historia nzuri na soka la Ulaya kufuatia kuwahi kufundisha Akademi ya FC Barcelona, anatarajia kukisimamia kikosi cha Young Africans kuweza kutimiza ndoto zake ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo.
Kwa sasa Young Africans imecheza michezo mitano ya Ligi Kuu, ikiwa na alama 13 kibindoni, imefunga mabao saba huku ikiwa imefungwa bao moja.