Kocha mkuu wa Young Africans Cedric Kaze amesema washambuliaji wa kigeni Yacouba Sogne na Michael Sarpong ni wachezaji wazuri, na usajili wao klabuni hapo aliupendekeza yeye kama kocha.
Washambuliaji hao kutoka mataifa ya Afrika Magharibi walisajiliwa Young Africans wakati wa dirisha kubwa la usajili mwezi Agosti, na tayari wameshafunga bao moja kila mmoja kwenye Ligi Kuu.
Kocha Kaze ambaye aliwasili nchini mwishoni mwa juma lililopita na kusaini mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi cha Young Africans, amesema anawafahamu vyema washambuliaji hao na ana matarajio makubwa kutoka kwao.
“Ngoja nikwambie kitu, Sarpong (Ghana) na Yacouba (Burkina Faso) wote ni washambuliaji wazuri, wanalijua goli vizuri tu, mimi ndiye nilipendekeza wasajiliwe baada ya kuwafuatilia muda mrefu.
“Lakini kilichotokea hadi wanaonekana wachezaji wa kawaida ni kwa sababu walikosa mbinu pamoja na viungo wa kuwawekea pasi za kufunga hali iliyosababisha hayo yote kutokea. Naamini ujio wangu utabadilisha kila kitu na mtauona ubora wao”.
Wakati huo huo Mkurungezi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said ameendelea kusisitiza sema kuwa watu ambao ana imani nao kubwa ni kocha mpya wa klabu ya Yanga Cedric Kaze.
Hersi amedai kuwa Kaze msimu huu lazima atawapa ubingwa hakuna kitu kingine wao kwa pamoja wanamwamini kocha huyo.