Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, Martha Koome amesema uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi wa Septemba 5, 2022 wa kuidhinisha kuchaguliwa kwa Rais mteule, William Ruto ilikuwa ni kazi ya Mungu.
Koome, ameyasema hii leo Septemba 7, 2022 wakati alipokuwa akiwahutubia waombolezaji kwenye ibada ya mazishi ya marehemu shangazi yake Bi. Salome Maingi Gakii, katika Kanisa la MCK Muiteria lililopo eneo la Imenti Kaskazini.
Amesema, “Hii hukumu ilikuwa ni kwa ajili ya uhuru wa taasisi, hasa Mahakama na haikutokana na nguvu au uwezo wetu kama Mahakama bali ni kwa sababu ya Mungu mwaminifu tunayemtumikia.”
Mahakama ya majaji saba, inayojumuisha Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu na Majaji, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola, Smokin Wanjala, Mohammed Ibrahim na William Ouko, kwa kauli moja ilitupa maombi ya Odinga kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Katika matokeo ya urais, Ruto alipata kura milioni 7.2 sawa na asilimia 50.49 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa Agosti 9, na sasa taratibu zinaandaliwa ilikuwezesha uapisho wake kama rais wa tano wa Kenya Jumanne ijayo Septemba 13, 2022.