Rais Mteulewa Kenya, William Ruto anatarajiwa kuapishwa siku ya Jumanne, Septemba 13, 2022 baada ya Mahakama ya Juu Zaidi kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa urais katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9.
Sherehe hiyo, inafanyika siku ya saba tangu tarehe ambayo Mahakama ya Juu zaidi imetoa uamuzi wake kutokana na kesi yoyote ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyowasilishwa huku wafuasi wa Ruto wakiendelea na shamrashamra za ushindi.
Tayari Rais, Uhuru Kenyatta amesisitiza kusimamia makabidhiano ya amani ya mamlaka kwa utawala ujao, na katika hotuba yake alisema atazingatia sheria na kuheshimu maamuzi ya michakato ya Mahakama wa kuidhinisha uchaguzi wa William Ruto kama Rais mteule.
Kwa upande wake, Raila Odinga amekubali uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi wa kuidhinisha uchaguzi wa Rais mteule William Ruto, lakini amesema kuwa hakubaliani na uamuzi huo na aliwataka wafuasi wake kudumisha utulivu wanapozingatia sheria.
Septemba 5, 2022, Mahakama ya juu nchini Kenya iliidhinisha Uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule baada ya kesi iliowasilishwa na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo Raila Odinga kukosa ushahidi wa kutosha.
Wakitoa uamuzi wao wa pamoja, majaji hao saba wakioongozwa na jaji mkuu, Martha Koome walisema kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa Raila Odinga ulikuwa umejaa uvumi na porojo.