Mahakama ya Juu imetupilia mbali ombi la kutaka kuzuia kuapishwa kwa rais mteule William Ruto, lililowasilishwa na wanaharakati 11 wakipinga uapisho wa Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua kushika wadhifa huo kwa madai ya kukosa uadilifu.
Mahakama hiyo ya upeo, ilisema haina mamlaka ya kushughulikia mambo yaliyoibuliwa na wanaharakati hao, na kwamba iliwafaa kuwasilisha kesi hiyo katika Mahakama Kuu.
Jana, Septemba 5, 2022 Mahakama hiyo ya juu nchini Kenya, iliidhinisha Uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule baada ya kesi iliyowasilishwa na mpinzani wake katika uchaguzi mkuu, Raila Odinga kukosa ushahidi wa kutosha.
William Ruto, anatarajiwa kuapishwa Septemba 13, 2022, huku Rais Uhuru Kenyatta kupitia hotuba yake akisitiza kusimamia makabidhiano ya amani kwa utawala ujao, na katika hotuba akisema atazingatia sheria na kuheshimu maamuzi ya Mahakama.