Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa jamii ya asili amepongeza uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu wa kuagiza serikali ya Kenya illipe fidia watu wa jamii ya asili ya Ogiek nchini humo kwa machungu na ubaguzi waliokumbana nao nchini humo.

 Kupitia taarifa, iliyotolewa jijini Geneva Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, mtaalamu huyo Francisco Cali Tzay, amesema uamuzi huo wa mwezi Mei mwaka huu unafuatia hatua ya mahakama hiyo kubaini kuwa serikali ya Kenya ilikiuka haki ya kuishi, kumiliki mali, maliasili, maendeleo, dini na utamaduni wa jamii ya Ogiek, kwa mujibu wa Katiba ya Mahakam ya Afrika ya Haki za binadamu.

Tzay amesema, uamuzi huo pamoja na malipo ya fidia ni hatua nyingine muhimu katika kutambuliwa na kulindwa kwa haki ya ardhi ya mababu za watu wa jamii ya ogiek kwenye msitu wa Mau nchini Kenya.

Jamii ya watu wa Kabila la Ogiek nchini Kenya.

Mahakama hiyo, imeitaka Serikali ya Kenya illipe fidia ya takribani dola 489,000 kwa kupotea kwa maliasili ya jamii hiyo na zaidi ya dola 844,000 kwa machungu waliyopitia kutokana na ubaguzi na kunyimwa haki ya maendeleo, utamaduni wao na dini yao.

Mahakama pia imetaka serikali ya Kenya ichukue hatua muhimu za kisheria, kiutawala au hatua zozote zile kutambua, kuheshimu na kulinda za waogiek iwe kwenye maendeleo, au uwekezaji wowote kwenye ardhi yao na wapatiwe haki ya kushirikishwa katika miradi yoyote itakayofanyika kwenye eneo lao.
 
Katika kesi hiyo, mtaalamu huyu wa Umoja wa Mataifa naye pia alitoa Ushahidi wa kitaalamu ambapo Tzay amesema, anapongeza sana uamuzi wa mahakama huku akisema unapeleka ujumbe mzito kwa ulinzi wa ardhi na haki za kitamaduni za waogiek nchini Kenya na watu wote wa jamii ya asili barani Afrika na kwingine kote duniani huku akitaka serikali ya Kenya itekeleze uamuzi huo.

Yusuph Mhilu: Ninarudi nyumbani
Mbunge arejesha furaha ya Wanafunzi ajali ya moto