Waziri wa Afya nchini Kenya, Cleopa Mailu amepiga marufuku uagizaji, utengenezaji utangazaji na uuzaji wa shisha nchini humo.
Nchi hiyo kwa sasa ni taifa la tatu kupiga marufuku shisha baada ya Tanzania na Rwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Dkt. Mailu ameonya kuwa mtu yeyote atakayekiuka sheria za udhibiti wa uvutaji wa shisha atapigwa faini isiopungua shilingi 50,000 za Kenya ama kifungo cha muda usiopungua miezi sita ama zote mbili kwa wakati mmoja.
Nchini Tanzania uvutaji wa Shisha ulipigwa marufuku kutokana na wasiwasi kwamba unahusishwa na dawa za kulevya na pombe.
Hata hivyo, Shirika la afya duniani hivi karibuni lilibaini kuwa uvutaji wa Shisha ni hatari kwa afya kwa sababu uvutaji wa sigara 100 hufanyika kwa awamu moja wakati mtu anapovuta shisha.