Aliyekuwa mwanasoka bora Duniani, George Weah ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais akipata asilimia 61.5 ya kura zote zilizopigwa na kuhesabiwa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia imemtangaza Weah aliyekuwa mgombea wa chama cha upinzani cha Democratic Change (CDC) kuwa amepata jumla ya kura 720,023, ikiwa ni kura 268,935 zaidi ya mpinzani wake Joseph Boakai wa chama tawala.

Matokeo hayo yanaanika wazi kuwa Weah ataapishwa kuwa Rais mpya wa Liberia akiwa mwanasoka wa kwanza nguli barani Afrika kuwahi kushika nafasi hiyo.

Weah atachukua nafasi inayoachwa na Ellen Johnson Sirleaf, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais katika taifa hilo na bara la Afrika, akifungua milango kwa mataifa mengine.

Mwanasoka huyo wa zamani ameweka wazi hisia zake kupitia mtandao wa Twitter, “ndugu zangu wa Liberia, kwa dhati natambua hisia za Taifa hili.”

Aliongeza kuwa anafahamu jukumu kubwa linalomkabili katika taifa hilo na kwamba muda wa mabadiliko umefika.

Tangu taarifa hizo zilipotolewa maelfu ya wafuasi wa Weah wameingia mtaani hususan katika jiji la Monrovia kusherehekea ushindi huo.

Familia ya Babu Seya yamsaka Magufuli
Kenya yafuata nyayo za Tanzania