Baadhi ya Wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwashirikisha wadau wa maendeleo waaminifu na wenye uwezo katika sekta ya maji, ili wawe kutoa huduma hiyo kiushundani na kuondoa adha ya uhaba wa hitaji hilo wanayokumbana nayo Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakizungumza katika maeneo tofauti ya jiji hilo hii leo Oktoba 30, 2022 wamesema, Serikali inapaswa kutafuta njia mbadala ikiwemo kuwashirikisha wadau hao kwani uhalisia unaonesha yapo mapungufu makubwa katika ufanikishwaji na utoaji wa huduma ya maji kwa Wananchi kitu ambacho kinapelekea wengi wao kuwa na wakati mgumu.

“Wasione aibu kama mambo yamewashinda kwa sasa Dunia ni kijiji waombe msaada kwa miji iliyoendelea nje ya nchi wapate wataalamu wawaelekeze wao waliwezaje kumaliza tatizo la maji, sababu haiwezekani miaka zaidi ya 60 ya uhuru eti bado wataalamu wetu wameshindwa kutafuta mbinu bora za ufanikishaji wa hitaji la maji,” amesema George Bega Mkazi wa Chanika.

Naye Salum Chilijila, mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni amesema, ni aibu kwa Taifa kubwa lenye historia nzuri Duniani likiwa na vivutio mbalimbali vya utalii na madini ya kila aina, kuwa na shida ya maji na mgao wa umeme na kwamba rasilimali zilizopo zinaweza kuinua nchi kiuchumi na kuweka misingi imara ya huduma za kijamii.

Amesema, “Matatizo yapo mengi na kila ukitafuta sababu unakosa kwani tumejaaliwa kila aina ya utajiri, kuna nchi zinalia zimezungukwa na maji ya bahari na pato lao kitaifa wanategemea uvuvi pekee tena ni nchi ndogo sana lakini wanatushinda sisi hii ni aibu kubwa sana Viongozi wetu wajitafakari kwanini tunazungumzia mgao wa maji hadi leo.”

Hta hivyo wameisisitiza Serikali kuacha kutegemea chanzo cha maji kimoja pekee kama ilivyo kwa mto Ruvu na badala yake watumie teknolojia kuhudumia maeneo yenye mito na maziwa yasiyo na huduma ya maji, na kwa jiji la Dar es Salaam, suluhisho la haraka ni kutoa maji Mto Rufiji na uchimbaji wa visima.

Hassan Dilunga: Mimi ni mwanafamilia Simba SC
Deo Kanda: Simba SC imetumia uzoefu