Mahakama Kuu, Dar es Salaam, imetengua hukumu iliyoiamuru kampuni ya simu za mkononi MIC (T) Limited, maarufu Tigo, kuwalipa wanamuziki wa kizazi kipya Hamisi Mwinyijuma (Mwana-FA) na Ambwene Yesaya (AY) Sh2.1 bilioni kwa kukiuka sheria za hatimiliki.
Jaji Joacquine De-Mello, amebatilisha uamuzi huo baada ya kukubaliana na rufaa ya Tigo kuwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala haikuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Hukumu na amri ya kuwalipa Mwana-FA na AY, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Juma Hassan, Aprili 11, 2016, kufuatia kesi ya madai waliyoifungua dhidi ya Tigo.
Hakimu Hassan aliridhika kuwa Tigo ilikiuka Sheria ya Hakimiliki na hakishiriki kwa kutumia kibiashara nyimbo zao ambazo ni ”Usije Mjini” na ”Dakika Moja” kama miito ya simu bila ridhaa wala makubaliano nao.
Jaji De-Mello, amekubaliana na hoja za Tigo iliyowakilishwa na wakili Rosan Mbwambo kuwa kiwango cha fidia cha Sh4.3 bilioni waliyokuwa wakiidai wasanii hao ni kikubwa kuliko uwezo wa kisheria wa mahakama hiyo.
Hata hivyo amesema kuwa kifungu cha 4 cha Sheria ya hakimiliki na hakishiriki kinatoa mamlaka ya masuala ya migogoro ya hakimiliki kwa mahakama za wilaya, lakini kwa kuzingatia ukomo mamlaka ya mahakama hizo kwa kiwango cha fedha katika shauri husika.
Kwa mujibu wa Gazeti la Mananchi Jaji De-Mello Amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 40 (1) (b) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, mahakama hizo zinapewa mamlaka yenye ukomo na hazipaswi kwenda zaidi ya mamlaka hayo.
Wakili wa kampuni ya Tigo, Rosan Mbwambo ameliambia Gazeti la Mwananchi kuwa atawaandikia barua wasanii hao kuwataka warejeshe fedha walizolipwa na mteja wake.
“Kama hawatafanya hivyo, tutafungua maombi ya utekelezaji ili tupate amri ya mahakama ya kukamata mali zao,” amesema wakili Mbwambo na kuongeza: “ikilazimu tutaiomba mahakama pia iamuru wafungwe.”
Wakati ikiwalipa fedha hizo, kampuni hiyo tayari ilikuwa imeshafungua maombi mahakama, ikiomba kibali cha kukata rufaa nje ya muda na baada ya kufanikiwa kupata kibali hicho ndipo ikakata rufaa hiyo.