Jebra Kambole ambaye ni wakili wa mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam, Abdul Nondo amesema leo mteja wake amepelekwa mahakamani, Wilayani Iringa, kufuatia kesi inayomkabili.
Lakini kesi hiyo imerushwa mpaka jumatatu ya tarehe 26, ambapo mahakama itaamua kumpa dhamana au kutompa dhamana.
Nondo amepandishwa kizimbani leo mbele ya Hakimu Mkazi, John Mpitanjia na kusomewa mashitaka mawili la kwanza likiwa la kuchapisha taarifa za uongo Machi 7, 2018 akiwa eneo la ubungo Dar es salaam na kuzisambaza kupitia mtandao wa kijamii wa wahatsapp akidai yupo hatarini.
Kosa la pili likiwa kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga alipokuwa anatoa taarifa kwa askari kwenye kituo cha polisi Mafinga na kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es salaam, na kupelekwa kiwanda cha Pareto Mafinga.
Hata hivyo Nondo amekana mashtaka hayo.
Aidha wakili wa utetezi, Chance Luwoga amesema mashtaka hayo aliyosomewa Nondo yanaruhusu kupewa dhamana hivyo haoni sababu ya kuizuia dhamana hiyo kwa mteja wake.
Kwa leo amerudishwa mahabusu kupitia sheria upya kuhusu dhamana yake.