Kiungo kutoka nchini Uganda na Klabu ya Young Africans Khalid Aucho amekanusha taarifa za kupokea ofa kutoka kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.
Aucho ambaye kwa sasa amekua gumzo kubwa kwa mashabiki wa soka nchini kufuatia uwezo wake wa kucheza soka, alitajwa kuhusishwa na mpango wa kuwaniwa na Simba SC wakati wa usajili kabla ya kuanza kwa msimu huu 2021/22.
Kiungo huyo amesema taarifa za kuwaniwa na Simba SC sio za kweli, na mara kadhaa amekua akisikia huo uvumi kutoka kwa wadau wengi wa soka nchini, lakini yeye kama muhusika anajua ukweli wa kila kitu.
“Nilikuwa nasikia Uvumi kwamba nilikuwa natakiwa na Simba, ukweli ni kwamba sikuwa na ofa yoyote na Simba na wala hakuna kiongozi wao ambaye alinipigia mimi na nikaongea naye,”
“Ukweli ni kwamba nilikuwa na ofa mbili tu Tanzania nilikuwaa nahitajika na Azam FC, niliongea nao na tukafikia sehemu lakini ya pili ni Injinia (Hersi Said), huyu ndiye niliyeongea naye sana na nikaona mambo yanakwenda sawa na mwisho tukakubaliana na nikaja kusaini hapa Young Africans,”
“Uamuzi wangu wa kuja Young Africans ulitokana na kuhitaji changamoto mpya ambayo niliiona hapa patakuwa sehemu sahihi kwangu.” amesema Aucho
Kiungo huyo amecheza michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Young Africans, na kuonesha msaada mkubwa katika eneo la kiungo, huku akisaidia kupatikana kwa ushindi kwenye michezo hiyo.