Kikosi cha Klabu ya Liverpool kimeeleza kushangazwa na namna ambavyo Ki-Jana Hoever mwenye umri wa miaka 16 tu alivyoweza kuonesha kiwango cha ajabu akimdhibiti mshambuliaji hatari Mohammed Salah kwenye mazoezi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Liverpol, mtoto huyo ‘Mdachi’ alipewa nafasi ya kucheza kwenye mazoezi ya klabu hiyo wiki moja kabla ya Krismas ili kuziba pengo la mabeki kadhaa wa timu hiyo waliokuwa majeruhi. Kocha Jurgen Klopp alimuweka Ki-Jana katikati ya msitu wa Simba washambuliaji kama Mo Salah.
Kiwango cha aina yake cha kuwadhibiti washambuliaji hao kilivuta usikivu wa kikosi hicho na kumshawishi Klopp kumpanga kwa mara ya kwanza katika mchezo wao dhidi ya Wolves katika kombe la FA.
Wachezaji wenzake walieleza kushangazwa na namna ambavyo alifanikiwa kumfanya Salah kuwa kimya hadi mwisho wa mchezo huo wa mazoezi licha ya kufanya jitihada za kutaka kupachika magoli.
-
Ronaldo kitanzini tena kwa ubakaji, polisi wataka vipimo vya DNA
-
Video: Ndege mpya ya sita kuwasili leo
Ki-Jana alionesha kiwango cha aina yake pia kwenye mechi hiyo ingawa timu yake iliambulia kichapo cha 2-1 dhidi ya Wolves lakini soko la Soka litakuwa limefunguliwa zaidi kwa ajili yake na thamani yake imepanda kwa kiwango kikubwa.
“Ni raha kumuangalia akicheza. Anajiamini na mchezaji mzuri sana. Ni furaha kuwa tunamuona siku hadi siku. Ni mchezaji bora wa siku za usoni, lakini hizo siku za usoni zinaanza lini hapo sifahamu,” alisema Klopp.
Mchezaji huyo kinda alihamia Merseyside akitokea Ajax katika msimu wa kiangazi, kwa kitita cha £90,000 lakini sasa amekua gumzo akisifiwa hata na wachezaji wakubwa wa Liverpool.
Ki-Jana anatarajia kufikisha umri wa miaka 17 wiki chache zijazo, na hapo atakuwa na uwezo wa kusaini mkataba kama mchezaji wa kulipwa, na tayari Anfield inaamini atakuwa almasi ya soka.
Ameweka historia ya kuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kupewa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool.