Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangalla amesema kuwa vurugu za uchaguzi zinazoendelea nchini Kenya zimegeuka kuwa neema kwa wadau wa utalii nchini ambapo wanadai kuwa idadi ya watalii imeongezeka kutokana na kuahirisha safari zao nchini humo.
Katika maonyesho ya siku tatu ya kimataifa ya utalii yanayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC), baadhi ya wadau wa utalii na mawakala wamesema kuwa idadi ya watalii imeongezeka kwasababu wanaogopa kwenda Kenya.
“Watalii wengi wanasema hupendelea kwenda Kenya kwa sababu ya miundombinu yao ni mizuri na unafuu wa gharama za utalii. lakini sasa wanahofia usalama wao kutokana na hali ya kisiasa iliyopo,” amesema Francis Lohay, mkuu wa fedha wa kampuni ya Bougain Villea Safari Lodge.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kitalii ya Patamu Lodge, Raymond Massae amesema kuwa sasa watalii hawapendelei kwenda Kenya, hivyo ni fursa kwa wadau wa ndani lakini Serikali inapaswa kuongeza utangazaji wa vivutio vya utalii na sio kutegemea anguko la wengine.
Aidha, mkurugenzi mtendaji wa Tanapa, Allan Kijazi amesema kuwa mapato yatokanayo na utalii kwa mwezi wa Julai na Agosti yamevuka lengo lililowekwa kwa asilimia saba hivyo idadi ya watalii imeongezeka.
- Video: Dkt. Mwakyembe aipongeza Kampuni ya DataVision Internatinal
- Ponda aendelea kushikiliwa na Polisi
- Aggrey Mwanri afuta likizo kwa watumishi
- Video: Sitafuta Mwenge kamwe katika uongozi wangu- JPM
Hata hivyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Khamis Kigwangala ameungana na wadau wa sekta ya utalii na kusema kuwa utalii nchini unakwenda vizuri kutokana na baadhi ya washindani kutokuwa na hali nzuri inayovutia kwa sasa.
“Watalii ni wengi mpaka hoteli zetu zinashindwa kuwamudu, hii ni kutokana na baadhi yao kuchagua kuja hapa na si kwa wenzetu. Sasa tunafanya uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza katika hoteli hususani za kitalii,” amesema Dkt. Kigwangala.