Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), imebainisha kuwa mwaka 2019, kila baada ya dakika 1 na sekunde 40 mtoto au kijana mwenye umri wa chini ya miaka 20 waliambukizwa Virusi vya Ukimwi na kuanya idadi ya watoto wanaoishi na VVU kufikia Milioni 2.8.
Ripoti hiyo iliyotolewa Novemba 25, 2020 mjini NewYork, Marekani na Johannesburg, Afrika Kusini imeeleza kuwa katika miezi ya Aprili na Mei, sanjari na kufungwa kwa mipaka, matibabu ya VVU kwa watoto na upimaji wa virusi kwa watoto katika nchi zingine ulipungua kati ya asilimia 50 hadi 70, na uanzishwaji mpya wa matibabu ulipungua kwa asilimia 25 hadi 50.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema bado hakuna chanjo ya VVU. “Watoto wengi wanaambukizwa kwa kiwango vya kutisha na wengi wanapoteza maisha kutokana na UKIMWI” amesema Henrietta.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo Ufikiaji wa akina mama wa tiba ya kurefusha maisha kuzuia maambukizi ya virusi kwa watoto wao, uliongezeka ulimwenguni hadi asilimia 85 na utambuzi wa mapema wa watoto ulifikia asilimia 60.
Idadi ya wanawake wajawazito wanaoishi na VVU ilikuwa milioni 1.3, watoto wanaokadiriwa kuwa 82,000 walio chini ya umri wa miaka mitano waliambukizwa wakati wa ujauzito au wakati wa kuzaa na 68,000 waliambukizwa wakati wa kunyonyesha.
Ripoti hiyo inazitaka serikali zote kulinda, kudumisha na kuharakisha maendeleo katika kupambana na VVU miongoni mwa watoto kwa kudumisha huduma muhimu za afya na kuimarisha mifumo ya afya.
Mwaka 2019 watoto 110,000 walifariki kwa UKIMWI.