Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania,Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kwa sasa akili zote ni kuelekea mchezo ujao wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Benin utakaofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Alkhamis (Oktoba 07).
Stars itashuka uwanjani kuwakabili Benin, ikiwa kileleni mwa Kundi J, ikiwa na alama nne baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mara moja.
Stars ililaizmishwa sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya DR Congo kwenye mchezo wa kwanza wa kundi J, huku ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Madagascar.
Kocha Kim amesema malengo ya kikosi chake ni kukusanya alama tisa katika ardhi ya nyumbani, wameanza na Madagascar sasa ni wakati wa kukusanya alama tatu dhidi ya Benin, licha kukiri kuwa atakutana na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wake hao.
“Tuko nyumbani tunaenda kujiandaa na mchezo unaofuata, ambao ni dhidi ya Benin tukiwa uwanja wa nyumbani tutapambana ili kuweza kupata nafasi ya kufuzu.”
“Kwa mchezo wetu uliopita ninawapongeza wachezaji kwa kuwa walipambana bila kukata tamaa, hivyo nina amini kwa mchezo ujao pia watafanya vizuri,” amesema Kim
Tangu jana Jumatatu (Oktoba 04) Taifa Stars imeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wao huo, ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu ikihitaji alama tatu muhimu.