Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesitisha shughuli za waganga wa kienyeji na kuwapiga marufuku kuwatibu watu, ikiwa ni hatua moja wapo za kupambana na kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola.
Watu 19 wamekwishakufa kutokana na Ebola katika mripuko mpya wa ugonjwa huo, wa kwanza tangu mwaka 2019. Aidha, Museveni amewaamuru maafisa wa usalama kuwakamata watu watakaokaidi kuwekwa karantini wanaposhukiwa kuwa na Ebola.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mkutano wa mawaziri wa afya wa nchi za kikanda kujadili hali ya mripuko wa Ebola ambapo visa 54 vya maambukizi ya Ebola vimekwishathibitishwa nchini Uganda tangu kuripotiwa ugonjwa huo katika wilaya ya Mubende.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameuarifu mkutano huo kwamba majaribio ya tiba dhidi ya aina ya Ebola inayosambaa Uganda yataanza mnamo wiki chache zijazo.