Katika jitihada za kukuza lugha ya Kiswahili barani Afrika, Tanzania imeziomba nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi na lugha ya kazi.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu, uliofanyika mjini Brazzaville wiki hii na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
“Tumewaomba wenzetu wa maziwa makuu wakubali lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha rasmi na lugha ya kazi katika nchi zote za maziwa makuu. Pia, nchi sita ambazo zipo hapa na hazijaridhia mabadiliko ya mkataba wa Afrika kuruhusu Kiswahili kutumika kama lugha rasmi katika Afrika (AU) nchi hizo zimetuhakikishia kuwa zitaridhia mabadiliko hayo ili kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaanza kutumika kama lugha rasmi ya kazi,” Alisema Dkt. Ndumbaro
Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda huo ni fursa ambayo italeta umoja wa kitaifa, na katika ukanda wa maziwa makuu lakini pia umuhimu wa Kiswahili kwamba ni lugha pekee ambayo haina uhusiano na ukoloni barani afrika.
“Tunatumaini kwamba tutazipata sahihi za nchi sita na tukishazipata tutabakiwa na sahihi ya nchi moja tu ili Kiswahili kiwe rasmi lugha ya kazi katika mikutano itakayokuwa inafanyika barani Afrika,” aliongeza Dkt. Ndumbaro
Nchi sita ambazo hazijaridhia mabadiliko ya mkataba wa Afrika kuhakikisha kuwa Kiswahili kinatumika kama lugha rasmi ya kazi ni pamoja na Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudani, Uganda na Zambia.
Kwa sasa hivi ni lugha rasmi lakini siyo lugha ya kazi kwa hiyo tumekwenda vizuri kwenye Kiswahili tunaamini ni fursa nzuri ya kuanza kukuza lugha ya Kiswahili katika bara la Afrika
Wakati huo huo, Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa, katika mkutano huo nchi wanachama waliweza kuongelea agenda kuu za nchi wananchama wa ukanda wa maziwa makuu ambazo ni Amani, Utulivu na Usalama hususani katika eneo la mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Sanjari na hilo, nchi nyingi zimeusifu uongozi wa Rais wa DRC, Felix Tshisekedi kuwa tangu alipoingia madarakani amejitahidhi kuhakikisha kuwa kuna kuwa na amnai ndani ya DRC pamoja na majirani zake. Pia Uganda, Rwanda pamoja na Angola zimesifiwa kufanikisha kusaini makubalianao ya kuleta amanai kati ya Uganda na Rwanda.
Akiongea awali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje Mgeni rasmi ambae alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Bwn. Clement Mouamba alisema kuwa mkutano wa leo, umelenga kuisaidia nchi ya DRC katika changamoto inazopitia hasa katika ukanda wa mashariki.
“Nawapongeza sana kwa kazi ambayo mmekuwa mkiifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa ugonjwa wa ebola unatokomezwa, kwani naamini kuwa umoja wetu tunaweza,” alisema Mouamba.
Aliongeza kwa kuzitaka nchi wanachama wa ukanda wa maziwa makuu kuendelea kulinda amanai na umoja walionao ili kuweza kuendelea na shughuli mbalimbali za maendeleo kwani bila amani ni vigumu sana kwa umoja huo kuendelea.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikianao wa Jamhuri ya Kongo, ambae pia alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo Mhe. Jean Claude Gakosso aliwasisitiza mawaziri wa nchi wanachama kuwa amani na umoja katika ukanda huo ni nguzo muhimu sana na hivyo waendelee kuishika amani hiyo.
Pia aligusia ugonjwa wa ebola na kuwataka nchi wanachama kutokata tama ya kupambana na ugonjwa huo licha ya changamoto zinazojitokeza.