Lori la mafuta lililoanguka na kulipuka karibu na soko la Onitsha katika jimbo la Anambra nchini Nigeria, limesababisha vifo vya watu watatu ikiwa ni pamoja na mama na mwanaye; na kuteketeza soko hilo pamoja na nyumba kadhaa.

Rais Muhammadu Buhari ameungana na wananchi kueleza masikitiko yao kutokana na vifo na uharibifu mkubwa wa mali uliotokea.

“Nimeguswa sana na ajali hiyo pamoja na vifo vya wananchi wasio na hatia wakiwemo mama na mwanaye ambao ni wahanga wa janga hili,” alisema Rais Buhari kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Garba Shehu.

“Pamoja na kueleza masikitiko yangu kuhusu janga hili, ni lazima niwatake wahusika hasa Mamlaka za Kiserikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha matukio haya yanayojirudia kwenye maeneo ya umma yanakoma,”aliongeza.

Lori hilo lenye tenki la mafuta lilianguka mtaroni karibu na kituo cha basi cha MCC, karibu na hospitali ya Toronto na soko la Onitsha.

Baada ya tenki hilo kuanguka, mafuta yalisambaa katika eneo lote na baadaye kulipuka. Moto huo ulisambaa na kuchoma nyumba kadhaa zilizokuwa barabarani na baadaye maeneo ya sokoni.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, moto huo uliteketeza nyumba sita na magari kadhaa.

Kiswahili chapendekezwa kutumika kama lugha rasmi ya kazi Ukanda wa Maziwa Makuu
Mmiliki wa Facebook aweka msimamo kuhusu zuio la siasa