Uongozi wa KMC FC umewataka wachezaji wote wa klabu hiyo kuripoti kambini leo Jumanne (Mei 25), kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC.
KMC ilitoa mapumziko kwa wachezaji wake kuanzia Mei 17 mpaka Mei 25 baada ya timu hiyo kutokuwa na mchezo wowote wa mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kwa muda wa mwezi mmoja.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya KMC FC Christina Mwagala, amesema: “Tulitoa mapumziko kwa wachezaji na tuliwaambia kwamba Mei 25 wanapaswa kurudi kambini. Kwa hiyo leo wanapaswa kurudi kambini na Jumatano tutaanza mazoezi mepesi.”
“Hii itakuwa maalumu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji ambao unatarajiwa kuchezwa Mei 17, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma,”
Kwenye msimamo wa ligi, KMC FC ipo nafasi ya 5 baada ya kucheza michezo 29 itakutana na Dodoma Jiji FC iliyo nafasi ya 8 na alama zao ni 39 baada ya kucheza michezo 30.
Timu hizo zilipokutana katika mzunguko wa kwanza Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, Desemba 4, KMC FC walichomoza na ushindi wa 1-0.