Rubani, Rudolf Erasmus wa nchini Afrika Kusini amelazimika kutua kwa dharura baada ya kugundua nyoka mwenye sumu kali aina ya kobra akiwa amejificha chini ya kiti chake.
Akiwa safarini, Rubani Erasmus na abiria wanne kwenye ndege ndogo amesema alihisi kitu baridi kikishuka kwenye sehemu ya chini ya mgongo wake na alipotazama chini kwa haraka na akaona kichwa kikubwa cha nyoka huyo aina ya Cape Cobra kikirudi uvunguni mwa kiti.
Msako wa Nyoka (Kobra), ndani ya Ndege ndogo iliyotua kwa dharula. Picha ya Brian Emmenis /AP.
“Ilikuwa kama vile ubongo wangu haukuwa ukitambua kilichokuwa kikiendelea, na baada ya kufikiri kwa haraka, niliwajulisha abiria wangu juu ya uvamizi wa nyoka huyo kikatokea kimya cha kushangaza japo niliwasihi watulie na tukafanikiwa kutua.” alisema Erasmus.
Hata hivyo, amesema alimpigia simu mdhibiti wa safari za anga ili kupata ruhusa ya kutua kwa dharura katika mji wa Welkom uliopo katikati ya nchi ya Afrika Kusini na alilazimika kuendelea kuruka kwa dakika nyingine kati ya 10 hadi 15 na kutua akiwa na nyoka amejikunja miguuni mwake.