Wakati Kikosi cha Azam FC kikianza safari ya kuelekea Benghazi-Libya tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Akhdar, Kocha Mkuu wa matajiri hao wa Chamazi Denis Lavagne ametoa kauli nzito.
Azam itaanzia ugenini Oktoba 8, mwaka huu na mchezo wa marudiano utakuwa nyumbani jambo lililompa nafasi kocha mkuu wa Matajiri hao wa Chamazi, Mfaransa kutumia uzoefu wake wa soka la Afrika kuwaondosha Walibya hao na kuendelea na michuano hiyo.
Kocha Lavagne amesema kazi kubwa wanayokwenda kuifanya Libya ni kupambana ili kupata matokeo, ambayo anaamini yatakisaidia kikosi chake kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mwishoni mwa juma lijalo Azam Complex-Chamazi, Dar es salaam.
Kocha huyo aliyewahi kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008 akiinoa Cotton Sports ya Cameroon na 2021 alipoifikisha JS Kabaiyle ya Algeria fainali ya Kombe la Shirikisho ameeleza kulijua vyema soka la Afrika na kuwasoma Al Akhdar, hivyo atatumia uzoefu wake kwenye mchezo wa Jumamosi (Oktoba 08).
“Tutahakikisha tunapambana ugenini dhidi ya wenyeji wetu Al Akhdar, najua mchezo hautakua rahisi kwa sababu soka la Afrika limegubikwa na mambo mengi ya ndani na nje ya Uwanja, lakini kazi inayotupeleka Libya ni kupambana na kupata matokeo.”
Zaka Zakazi apigwa mvua ya miezi mitatu
“Naamini mambo yakitunyookea ugenini, tukirudi hapa tutakuwa na nafasi nzuri ya kumalizia pale tutakapoishia ugenini, nimewaandaa vizuri wachezaji wangu kuelekea mchezo wetu dhidi ya Al Akhdar, nasisitiza tutapambana na kupata matokeo ugenini.” amesema kocha huyo
Kikosi cha wachezaji 25 wa Azam FC kimeanza safari ya kuelekea jijini Benghazi-Libya leo Alhamisi (Oktoba 06) saa 11.25 Alfajiri, huku mchezo dhidi ya Al Akhdar ukipangwa kucheza keshokutwa Jumamosi (Oktoba 08) majira ya saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.