Mahakama ya Rwanda siku ya Jumatano iliwaachilia huru wanahabari watatu waliokuwa wamezuiliwa kwa miaka minne kwa madai ya kueneza habari za uwongo na kushtakiwa kwa kuchochea uasi, kueneza habari za uongo kwa nia ya kujenga maoni ya kimataifa yenye uadui kuhusu Rwanda na kuchapisha taarifa na picha ghushi.

Wanahabari hao watatu, Damascene Mutuyimana, Shadrack Niyonsenga na Jean Baptiste Nshimiyima walikamatwa Oktoba 2018 wakati wa msako dhidi ya WanaYouTube wa kituo cha mtandao wa Iwacu TV, waliokosoa serikali ya Rais Paul Kagame lakini mahakama mjini Kigali imewaondolea mashtaka yote, baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.

Mahakana hiyo imesema, “Kile ambacho upande wa mashtaka uliwasilisha hakikutosha kama ushahidi katika uhalifu ambao washtakiwa watatu wanatuhumiwa… lazima waachiliwe.” na hukumu hiyo ilitoka bila ya Wanahabari hao kuwapo mahakamani na Wakili wao Jean Paul Ibambe alionesha kufurahia hukumu hiyo.

Wakizungumzia hukumu hiyo, baadhi ya Wanaharakati wa haki walisema ushindi umekuja kwa kuchelewa, wakibainisha kuwa washtakiwa walikuwa tayari wamekaa gerezani kwa miaka minne na kusema “Mfumo wa haki unahitaji kuanza kuzingatia masuluhisho mengine kama vile dhamana kwa sababu kukaa jela miaka minne kwa makosa ambayo hukufanya ni dhuluma.”

Mkurugenzi wa Afrika ya Kati wa Human Rights Watch, Lewis Mudge amesema “Afueni ya kuachiliwa kwa wanahabari hao watatu imegubikwa na kushindwa kwa mahakama kusitisha udanganyifu huu wa kesi mapema na hukumu hii itatuma ujumbe wa kutia moyo kwa wengine ambao wanathubutu kutumia haki yao ya kujieleza nchini Rwanda.”

Rwanda, iliyotawaliwa na Kagame tangu mwisho wa mauaji ya kimbari ya 1994 yaliyosababisha vifo vya Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani, mara nyingi imekuwa ikishutumiwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kukandamiza uhuru wa kujieleza, wakosoaji na upinzani.

Watu kadhaa wameikosoa mamlaka ya Rwanda baada ya kugeukia YouTube ili kuchapisha maudhui yanayoikosoa serikali ya Kagame, ambapo Dieudonne Niyonsenga, anayejulikana zaidi na mtu wake wa YouTube Cyuma (“Iron”), alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela Novemba mwaka 2021, baada ya kupatikana na hatia ya kughushi na uigaji wa maudhui.

Kufungwa kwake kulikuja wiki kadhaa baada ya nyota mwingine wa YouTube, Yvonne Idamange, kufungwa jela miaka 15 kwa kuchochea vurugu mtandaoni huku nchi hiyo ikiorodheshwa na shirika la uangalizi wa vyombo vya habari la Reporters Without Borders, kuwa ya 136 kati ya nchi 180 kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Walimu waboreshewe stahiki uinuaji sekta ya Elimu
Kocha Azam FC ategemea ushindi Libya