Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Prisons, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema kasi waliyonayo sasa ya kushinda mechi mfululizo ndiyo watakayoanza nayo katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Bares aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Aprili anesema Prisons ni timu kongwe nchini na wanahitaji kufanya vizuri hivyo watahakikisha kasi wanayomaliza nayo ligi sasa ndiyo watakayoanza nayo msimu ujao na kuwa tishio.
“Wengi wanaifahamu Prisons ni timu kongwe Tanzania, lakini nafikiri ni upepo mbaya tu ulimpitia mtangulizi wangu (Patrick Odhiambo) na nimeyaona machache nimeyafanyia kazi, vijana wamebadilika, tunataka hiyo kasi tunayomaliza nayo ndiyo tutakayoanza nayo msimu ujao,” amesema Bares.
Bares aliyeanza kuinoa Prisons Februari, mwaka huu akitokea Mlandege ya Zanzibar amesema Ligi Kuu Bara imeonesha kuimarika ndio maana kuna timu nyingi zinapata shida kwenye mabadiliko hayo ya ugumu wa mechi lakini anaamini ataitengeneza Prisons katika ushindani huo msimu ujao.
Prisons ilikuwa ikiyumba kabla ya sasa kushinda mechi mfululizo na kushika nafasi ya nane kwa alama 34 ikiwa imeshinda mechi nne mfululizo.