Wakati Tetesi zikiendelea kusambaa kuhusu usajili wa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza kusajiliwa Simba SC kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili, Kocha Msaidizi wa Geita Gold FC Mathias Wandiba amebadili upepo wa taarifa hizo.
Saido alisajiliwa Geita Gold FC mwanzoni mwa msimu huu akiwa mchezaji huru, kwa lengo la kuisaidia Klabu hiyo ya Mkoani Geita katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, lakini ilishindikana kufuatia jina lake kutowasilishwa CAF kwa wakati.
Kocha Wandiba amezungumza na Waandishi wa Habari mjini Geita akisema taarifa za Kiungo huyo kusajiliwa Simba SC hawazitambui na hadi sasa Saido ni mchezaji halali wa Geita Gold FC.
“Kikubwa suala Saidoo sio jukumu langu sana kulizungumzia mimi mpaka sasa hivi ni kama mwalimu na bado nategemea kwamba ni mchezaji wetu kwa sababu hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa uongozi iliyokamilika” alisema Wandiba
Juma lililopita Kocha Mkuu wa Geita Gold FC Fred Felix Minziro alikaririwa na baadhi ya vyombo vya Habari akimtakia kila la kheri Saido katika maisha yake mapya, japo hakuweka wazi wapi atakapoelekea katika Kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili.