Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes, amesema itamlazimu kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha ushindi dhidi ya Young Africans, Jumamosi (Mei 08) ili kukaribia lengo la kutetea ubingwa wa VPL msimu huu 2020/21.
Simba watakuwa wenyeji wa Young Africans katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku mashabiki wa soka nchini kote wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Novemba 7, mwaka 2020.
Kocha Gomes amesema: “Tumefurahi kwa ushindi ambao tuliupata katika mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar katika michuano ya Kombe la FA, kwa sasa tunajua tuna ratiba ya kucheza michezo mikubwa dhidi ya Yanga na michezo ya robo fainali ya mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs.
“Lakini mawazo yetu yote tumeyaelekeza kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Yanga, kwa kuwa ni mchezo mgumu wa dabi, nafurahi kuona kuelekea mchezo huo tupo katika hali nzuri ya kujiamini kutokana na kupata ushindi katika michezo yetu sita iliyopita.
“Narudia tena tunajua wazi utakuwa mchezo mgumu, lakini tunataka kushinda mchezo huo kwani ni wazi kama tutashinda mchezo huo basi kwa asilimia 100 tutakuwa mabingwa msimu huu.
“Kuhusu kiwango bora cha Morrison, nadhani kila mmoja anajua kuwa ni mchezaji mzuri na anatufaidisha kwa vitu vingi uwanjani, kwenye michezo miwili iliyopita ametimiza vizuri majukumu yake ya kuhakikisha anatoa presha kwa wapinzani, siwezi kuhakikisha uwepo wake katika mchezo dhidi ya Yanga lakini tunamhitaji hata tunapokutana na safu ngumu ya ulinzi,”
Mpaka sasa Simba ndiyo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo wamejikusanyia alama 61, wakifuatiwa na Young Africans wenye alama 57, licha ya kwamba wamecheza michezo miwili zaidi ya Simba.