Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Tanzania) wameitangazia vita Polisi Tanzania FC kuelekea mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
JKT Tanzania wametangaza vita dhidi ya maafande wenzao kutoka mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya kutaka kurejesha heshima ya kupata alama tatu, baada ya kuzipoteza mbele ya Dodoma Jiji FC kwa kufungwa mabao 2-1 mwishoni mwa juma lililopita.
Kuelekea mchezo huo, Mkuu wa Benchi la Ufundi la JKT Tanzania FC Abdalah Mohamed ‘Bares’ amesema wanaupa umuhimu mkubwa mchezo wa leo, kutokana na hitaji la alama tatu muhimu.
Amesema wanaamini endapo watapata alama tatu za mchezo wa leo dhidi ya Polisi Tanzania, itawasaidia katika mbio za kufikia lengo walilojiwekea msimu huu wa 2020/21.
“Bado hatujaka tamaa kwenye michezo yetu kwa kuwa mzunguko wa kwanza kuna mapungufu ambayo tulikuwa nayo na tumeyafanyia kazi hivyo kwa mzunguko wa pili tuna amini tutafanya vizuri zaidi, mashabiki watupe sapoti.” Amesema Bares.
“Leo tunakwenda kucheza dhidi ya Polisi Tanzania, tumejipanga kupambania alama tatu muhimu, sina shaka na hilo kwani maandalizi nilioyafanya yatatuwezesha kufanikisha hitaji letu.” Amesema kocha huyo kutoka visiwani Zanzibar.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara JKT Tanzania ipo nafasi ya 14 ikiwa imekusanya alama 20 baada ya kucheza michezo 19, huku Polisi Tanzania ikiwa nafasi ya 10 na alama 23.