Kocha Mkuu wa Young Africans Cedrick Kaze, ameweka hadharani mbinu alizozitumia kuiadhibu Azam FC kwenye mchezo wa mzunguuko wa 12 wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana Jumatano usiku, Azam Complex Chamazi.
Kocha Kaze amesema ilimlazimu kutumia mbinu mbadala ambazo zilifanikisha lengo la kupata alama tatu muhimu ugenini, zilizowapeleka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 28.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema haikua kazi rahisi kufanikisha ushindi walioupata kwa mbinu alizozibuni kwenye mchezo huo, ambao ulikua na ushindani mkubwa.
“Ulikuwa ni mchezo ambao unahitaji ushindani mkubwa na wachezaji wenye spidi kubwa ili kuwachosha wachezaji wa timu pinzani kwa sababu wengi wao ni wazito.”
“Nilipaswa kuwa na mbinu ambayo ingenipa matokeo nikaanza na Kaseke ambaye alifunga bao na kutupatia alama tatu, katika hilo ninawapongeza wachezaji wote kiujumla pamoja na mashabiki.” Amesema Kaze.
Bao la Young Africans lililofungwa na kiungo mshambuliaji Deus Kaseke dakika ya 48 lililodumu mpaka dakika ya 90 na kumshinda mlinda mlango David Kissu.
Bao hilo linakua la kwanza kwa mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Mbeya City na Singida United kwa msimu huu, na kuiwezesha Young Africans kupanda kwenye nafasi ya kwanza kwa kuishusha Azam FC inayonolewa na kocha Mromania Aristica Cioaba.
Young Africans inakuwa imecheza jumla ya michezo 12 ambayo ni sawa na dakika 1,080 bila kufungwa, huku Azam FC ikipoteza mchezo wa tatu baada ya kucheza michezo 12 ipo nafasi ya pili.
Wakiwa nafasi ya tatu, Mabingwa watetezi Simba SC wana alama 23 baada ya kucheza michezo 11 imepoteza michezo miwili dhidi ya Tanzania Prisons kwa kufungwa bao moja kwa sifuri, na ule dhidi ya Ruvu Shooting kwa kufungwa bao moja kwa sifuri.